SOMO: VIFO VYA KUTENGENEZA

SOMO: VIFO VYA KUTENGENEZA
SNP: PAUL JOSHUA
Ni kweli watu wanakufa na kuna vifo ambavyo ni mpango wa Mungu lakini kuna asilimia kubwa ya watu ambao wanaokufa; na vifo hivyo vinakuwa ni vifo vya kutengeneza. Mtu anapozaliwa Mungu anampa miaka mingi ya kuishi lakini hapa katikati wachawi wanatokea wanatengeneza matukio ili kufupisha maisha yako. Yawezekana umetengenezewa kifo kwenye ukoo wako au kwenye familia yako na kabla hakijakupata leo tunaibomoa kwa jina la Yesu.

MATHAYO 27:1 Na ilipokuwa asubuhi, wakuu wa makuhani wote wa wazee wa watu wakafanya shauri juu ya Yesu wapate kumwua.

Tunaona kikao cha wazee kinaandaa mauti juu ya Yesu, kumbe watu wanaweza kukukalia kikao ama usiku ama mchana wakaandaa kifo kwenye maisha yako. kwa maana kila tukio baya linalokutokea wewe kuna sehemu limetokea hakuna tukio linakuja kwako kwa bahati mbaya. Matukio yote mabaya yanatengenezwa kuzimu, na mazuri yanatengenezwa mbinguni; na leo tunaamuru mbingu itengeneze mambo mazuri kwaajili yako, kwaajili ya familia yako kwa jina la Yesu.
Wazee wakaona kati ya wanafunza kumi na mbili wa Yesu kuna mtu ambaye watamtumia ili kumwangamiza Yesu, Yuda akaitwa akaambiwa unataka shilingi ngapi akasema nataka vipande ishirini vya fedha.

Kuna kundi la watu wamekaa kikao ili kutengeneza kifo kwaajili yako lakini leo kabla hujalia wewe watalia wenyewe. Maana Yuda aliyemsaliti Yesu kabla Yesu hajafa Yuda akajinyonga, msalaba ambao aliuandaa Hamani ili kumtundika Morkedai akatundikwa yeye; na leo kila aliyekaa kikao kuandaa kifo juu ya maisha yako kiwarudie wenyewe; maana imeandikwa anayepolomosha jiwe kwaajili yako limrudie mwenyewe, anayekuchimbia shimo atatumbukia mwenyewe.

UKiri: Kwa damu ya Yesu ninabomoa kila uchawi uliotumwa kwenye familia yangu roho za kifo ninazibomoa kwa jina la Yesu, hakuna kifo kwenye familia yangu, kwenye nyumba yangu, kwenye ndoa yangu, kwa watoto wangu, ninakataa kwa jina la Yesu.
Adui zako waache waje maana wanakutengenezea mafaninikio, ili ushindi uje kwenye maisha yako ni lazima Yuda awepo ili akutengenezee mazingira uinuke. Yule adui yako ni daraja la ndoa yako, ni daraja la huduma yako, na ukimuona adui yako mwambie wewe ni daraja langu bila wewe sitaweza kupiti.

Usiogope kwaajili yao kwa maana wao wanataja magari, wao wanataja farasi, wao wanataja waganga wa kienyeji, lakini sisi tunalitaja jina la BWANA. Ni kweli wanashindana nasi lakini hawatashinda maana walio upande wetu ni wengi sana kuliko walio upande wa adui zako.
Anayeaandaa kikao kwaajili yako ni daraja la maisha yako bila yeye huwezi kupita, wamekaa vikao wanajadili utakufa lini? Imeandikwa Sitakufa bali nitaishi hadi niyasimulie matendo makuu ya BWANA hautakufa kwa damu ya mwana kondoo.
Inawezekana kuna wazee wa mtaa wamekaa sehemu ili kujadili ndoa yako, kujadili masomo yako, kujadili kazi yako, lakini imeandikwa vita si vyako bali ni vya BWANA nyamazeni kimya muone BWANA atakavyowapigania wamisri mnaowaona leo hamtawaona tena maadui zako walioinuka leo hutawaona tena.

Kifo kinaweza kutengenezwa kwa njia ya ajali; kwa maana hakuna dereva anayependa kufa, au hakuna bodaboda anayependa kufa hata kama ni mlevi. Lakini wachawi wanaweza kutengeneza kifo cha ajali; wanaweza wakaita majini jini makata, jini subiani, wanatoa kafara ya damu wanayapa majini wanayaambia kaa barabarani ili mtu Fulani anapokuja umtie kizungu-zungu anguke.
Kifo kinaweza kutengenezwa kwa namna ya magonjwa. Kuna kiwanda sehemu cha kutengeneza magonjwa, na ukitaka kutoka kwenye magonjwa tafuta kiwanda cha kutengeneza magonjwa, maana siyo kila mwenyeugonjwa ni wa kawaida,siyo kila Ukimwi ni wa kawaida, unaweza kutengenezewa. Unaweza ukaenda kupima ukaambiwa una sukari au unaambiwa moyo umepanuka kumbe yanakuwa ni magonjwa ya kutengeneza.
Hata kwenye familia mnaweza kutengenezewa magonjwa unakuta kila mwaka lazima afe mtu, wengine unakuta kwenye familia kuna ugonjwa wa presha, ugonjwa wa moyo, sasa leo kile kifo ambacho kimetengenezwa kikupate, wewe au familia yako au watoto wako tunakibomoa kwa jina la Yesu.

DANIEL 6:1-7 Ilimpendeza Dario kuweka juu ya ufalme maliwali mia na ishirini, wawe juu ya ufalme wote na juu yao akaweka wakubwa watatu, na Danieli alikuwa mmoja wao, ili maliwalo hao watoe hesabu kwao mfalme asipate hasara. Basi Danieli huyo alipata sifa kuliko wakubwa na maliwali, kwakuwa roho bora ilikuwa ndani yake; naye mfalme akaazimu kumweka juu ya ufalme wote. Basi mawaziri wakatafuta sana kupata sababu za kumshitaki Danieli kwa habari za mambo ya ufalme lakini hawakuweza kuona sababu wala kosa; kwa maana alikuwa mwaminifu wala hakuonekana kosa wala hatia ndani yake. Ndipo wale watu wakasema hatutapata sababu ya kumshitaki Danieli huyo tusipoipata katika sheria ya mambo ya Mungu wake. Basi wale mawaziri na maamiri wakakusanyika pamoja mbele ya mfalme wakamwambia hivi mfalme Dario uishi milele. Mawaziri wote wa ufalme na manaibu na maamiri na madiwani na maliwali wamefanya shauri pamoja ili kuweka amri ya kifalme na kupiga marufuku ya kwamba mtu yeyote atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote au kwa mtu awaye yote katika muda wa siku thelasini ila kwako Ee mfalme atatupwa katika tundu la simba.
Tunawaona hawa walifanya shauri kwaajili ya Danieli ili kuandaa kifo kwaajili yake, muda mwingine inawezekana Mungu amekuinua mahali pako pa kazi adui zako wanaamua kufanya shauri ni jinsi gani wakuangamize. Lakini usiogope Mungu yuko pamoja nawe hakuna jambo lisilowezekana kwake, watafanya sana mashauri lakini hayatafanikiwa kwa jina la Yesu.
Usiogope adui zako wewe songa mbele utafanikiwa mbele ya macho yao; adui yako ni daraja lako na ukitaka upite tafuta adui, ukimuona adui amekuja kwako ujue kuna hatua nyingine kwenye maisha yako. Hao wamisri unaowaona leo hautawaona tena maana BWANA atakupigania f-Farasi na mpanda Farasi BWANA amewatosa baharini, leo adui zako tunawatosa ziwa Tanganyika kwa jina la Yesu.

Unapoona jambo limekutokea iwe kwenye ndoa ama kwenye huduma kuna sehemu kikao kimekaliwa, tafuta kikao kilipokaliwa usihangaike na magonjwa tafuta kiwanda cha magonjwa tunazifuata kwenye ulimwengu wa roho na kukipasua kwa jina la Yesu.
Kunapokuwa na watu wanakutafuta lazima Yuda awepo, mtu anayekujua vizuri ni lazima awepo ili kuwaambia latiba zako huwa zinaendaje, anakuwa anakujua unatoka saa ngapi na unarudi saa ngapi na unapita njia ipi, lakini leo tunatuma malaika kwenye kila hatua zako wakutangulie unapopanda gari na kila unapokanyaga nyayo za miguu yako. Wanatega mitego mauti ikupate popote ulipo siyo wewe tu hata wanao lakini kwakuwa umeokoka neema yako yatosha kuwafunika ndugu zako na watoto wako hata kama hawajaokoka.

Dalili za kujua kama kuna roho ya kifo au mauti imetumwa kwako, au kwenye familia yako.
1. Kuota ndoto za msiba; tambua kuna jambo baya ambalo limetumwa lije kwenye maisha yako au kwenye familia yako.
2. Kuota unalia; tambua kuja jambo baya limepangwa lije likulize.
3. Kukosa amani; yaani siku nzima hauna amani, unalala usingizi unaota ndoto mabaya, unashangaa mbona sina amani leo hiyo ni ishara kuna roho ya kofo ama kwenye familia.
4. Moyo kushituka-shituka. Unatembea unawaza kifo, Ndio maana mtu aliyeokoka mmoja anaweza kuzuia mauti kwenye familia nzima.
Ukiri: kwa damu ya Yesu roho ya kifo iliyotumwa kwangu au kwenye familia yangu ninaivunja kwa jina la Yesu, nakataa kifo kwenye maisha yangu kwa jina la Yesu, nakataa kifo kwenye familia yangu, kwenye ukoo naibomoa roho ya kifo kwa jina la yesu.